Wednesday, October 21, 2009

NI USIKU WA MAAJABU ULIKUWA JANA BARANI ULAYA!!!
MASKINI: Liverpool ni vipigo mfululizo!!!! Barca waaibishwa Nou Camp!!!
echi za jana za UEFA CHAMPIONS LEAGUE zimeleta matokeo yasiyotarajiwa na magoli bwelele huku ajabu kubwa ni pale Warusi Rubin Kazan walipowakung’uta Mabingwa Watetezi wa Ulaya FC Barcelona kwa bao 2-1 tena wakiwa nyumbani kwao Nou Camp.

Liverpool wameendelea kupata vipigo mfululizo ingawa jana sio puto ndio liliwafunga bali ni goli la dakika za majeruhi wakiwa kwenye ngome yao Anfield na pia kupata athari kubwa pale mhimili wao na Nahodha wao Steven Gerrard kucheza dakika 25 tu za mwanzo na kulazimika kutoka baada ya kuumia.
Matokeo ya mechi ya jana ambayo Liverpool alifungwa 2-1 na Lyon ya Ufaransa yamedhihirisha ile imani ya wengi kuwa Liverpool bila Gerrard na Torres ni nyanya tu. Jana Torres hakucheza kabisa.
Sasa, baada ya vipigo mfululizo, Jumapili kwenye Ligi Kuuu, Liverpool wanawakaribisha Mahasimu wao wakubwa Manchester United na hilo linawatia homa Mashabiki wa Liverpool.
Arsenal wakiwa ugenini huko Uholanzi na huku wakiongoza bao 1-0 walilazimishwa sare ya 1-1 na AZ Alkmaar.
Rangers ya Scotland iliadhiriwa vibaya ikiwa nyumbani baada ya kuchapwa bao 4-1 na Unirea Urziceni.
Sevilla, baada ya mechi 3 tu, wameweka rekodi huko Ulaya baada ya kufuzu kusonga mbele Raundi nyingine baada ya mechi 3 tu.
Matokeo kamili mechi za jana Jumanne, Oktoba 20:
KUNDI E
Liverpool 1 Lyon 2
Debrecen 3 Fiorentina 4
KUNDI F
Inter Milan 2 Dynamo Kiev 2
Barcelona 1 Rubin Kazan 2
KUNDI G
Stuttgart 1 Sevilla 3
Rangers 1 Unirea Urziceni 4
KUNDI H
AZ Alkmaar 1 Arsenal 1
Olympiakos 2 Standard Liege 1

No comments:

Post a Comment