Saturday, September 12, 2009

FIFA yaizuia Chelsea kuwarudisha hata Wachezaji wao waliowatoa kwa mkopo!!

FIFA imewaambia Chelsea hawaruhisiwi kuwarudisha Wachezaji wao waliowatoa kwa Klabu nyingine kwa mkopo wa msimu mzima kufuatia kifungo chao cha kutosajili Wachezaji kwa vipindi viwili vya usajili ikimaanisha hawawezi kusajili hadi mwaka 2011 adhabu ambayo wamepewa baada ya kumchukua Chipukizi Gael Kakuta kutoka FC Lens ya Ufaransa kinyume cha taratibu.Ingawa Chelsea wana nia ya kukata rufaa kupinga adhabu hiyo, Meneja wao Carlo Ancelotti alitaka kupunguza makali ya adhabu hiyo kwa kuwarudisha Wachezaji wao Klabuni waliowatoa kwa mkopo akiwemo Mchezaji wa Timu ya Vijana ya England wa chini ya miaka 21 Michael Mancienne kutoka Wolves, Scott Sinclair toka Wigan na Muargentina Franco di Santo kutoka Blackburn.FIFA imetoa ufafanuzi kuwa ni Di Santo pekee anaeweza kurudi Stamford Bridge kwa vile mkopo wake ni nusu msimu lakini Sinclair haruhusiwi kurudi kwa vile mkopo wake ni wa msimu mzima na kuhusu Mancienne, ingawa mkopo wake ni wa msimu mzima, FIFA itatoa uamuzi baadae kuhusu kipengele cha mkataba ambacho kinatamka anaweza kurudi Chelsea kwa dharura.Mpaka sasa Chelsea wanangoja kupokea kutoka FIFA adhabu yao rasmi ndani ya siku 10 zijazo na kisha wanatakiwa ndani ya siku 21 kukata rufaa.Chelsea wametaka kuwarudisha Wachezaji hao iliowatoa kwa mkopo ili wawe kava ya akina Didier Drogba, Michael Essien, John Obi Mikel na Salomon Kalou ambao itawakosa mwezi Januari 2010 kwani wote wanategemewa kuwakilisha Nchi zao kwenye mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika huko Angola.Hata hivyo Januari 2010, Chelsea wanategemea majeruhi wao wa muda mrefu Paulo Ferreira na Joe Cole kurudi uwanjani baada ya kupona magoti waliyoumia.

No comments:

Post a Comment