Saturday, September 12, 2009

Wenger akiri: “Ni muhimu kumsimamisha Adebayor!”

Arsene Wenger amekiri kuwa ili Timu yake Arsenal iambulie chochote kwenye mechi ya leo ya Ligi Kuu England watakapocheza City of Manchester City Stadium na wenyeji Manchester City ni muhimu kumkaba Emmanuel Adebayor alieihama Arsenal na kwenda Man City msimu huu kwa vile ndie anaeng’ara sana kwa sasa.Adebayor msimu huu, katika mechi 3 za Man City Ligi Kuu ambazo wameshinda zote, amefunga goli katika kila mechi.Wenger vilevile ameongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni Mchezaji pekee ambae kiwango chake kilipanda juu sana kwa muda mfupi ni Adebayor ambae alimnunua kutoka Monaco mwaka 2006.Wenger amesema: “Tulimchukua kutoka Monaco akiwa hana namba huko na alipokuja kwetu kiwango chake kilipanda sana! Tunafurahia yote aliyotufanyia Arsenal na nadhani Klabu zote mbili, Arsenal na Man City, zimeridhika! Sisi tumepata pesa nzuri na wao wamepata Straika bora!”Mbali ya Adebayor, Man City pia imemchukua msimu huu Mlinzi Kolo Toure kutoka Arsenal ambae pia anang’ara na Timu yake mpya akiiongoza ngome ambayo katika mechi zao 3 za Ligi Kuu hawajafungwa hata goli moja.
Katika mechi ya leo, Man City itawakosa nyota wao Robinho na Tevez ambao wote waliumia katika mechi moja wakati Nchi zao Brazil na Argentina zilipokutana kwenye mechi ya Kombe la Dunia Jumamosi iliyopita huko Rosario City, Argentina na Brazil kushinda 3-1.
Arsenal watamkosa majeruhi Andriy Arshavin lakini Nahodha wao Cesc Fabregas na Tomas Rosicky wapo fiti na huenda wakacheza.
Mechi kama hii msimu uliokwisha, Man City walishinda bao 3-0.
Refa katika mechi ya leo ni Mark Clattenburg.


No comments:

Post a Comment