Saturday, September 5, 2009

Chelsea yapata matumaini kidogo toka CAS, Mahakama ya Usuluhishi Michezoni!!!!

Huenda Chelsea wakaruhusiwa kusaini Wachezaji wapya wakati Dirisha la Uhamisho likifunguliwa tena Januari 2010 mbali ya kuwa kifungoni hadi 2011 kutosajili Mchezaji kwa kukiuka sheria za usajili walipomchukua Chipukizi Gael Kakuta toka FC Lenz.Matumaini hayo yamekuja baada ya ufafanuzi kutoka CAS [Mahakama ya Usuluhishi Michezoni] kwamba endapo Chelsea watachelewesha kukata rufaa kwao na kuutumia muda wote wa kuwasilisha rufaa ndani ya siku 21, Mahakama hiyo itabidi icheleweshe kusikilizwa kesi hiyo na pia kuchelewa kutolewa uamuzi.Kawaida wakati Timu inapokata rufaa kwa CAS adhabu yao husimamishwa hadi uamuzi utolewe.Katibu Mkuu wa CAS, Mathieu Reeb, ametoa ufafanuzi: “Inategemea lini Chelsea wanakata Rufaa. Wakikata Rufaa wiki hii au ijayo, basi sisi tutapanga kusikiliza kesi Novemba na Desemba uamuzi utatoka. Lakini wakichelewesha na kutumia karibu siku zote 21 za kukata rufaa baada ya kupewa adhabu na FIFA, na sisi tutachelewa kuisikiliza na pengine kuto uamuzi baada ya Januari, 2010 na hivyo Chelsea wanaweza kusajili Januari, 2010 kwani kawaida adhabu husimama hadi uamuzi wetu.”Klabu ya Uswisi FC Sion ilikumbwa na mkasa kama wa Chelsea pale ilipomsajili Kipa wa Misri Essam El Hadary aliekuwa akichezea Al-Ahly na ikafungiwa kusajili na FIFA mwezi Aprili mwaka huu hadi 2010 lakini ikakata rufaa CAS na msimu huu imeruhusiwa kusajili kwani uamuzi wa rufaa yao utatoka baadae mwaka huu.Kawaida jopo linalosikiliza Rufaa huko CAS huwa na Majaji wawili, mmoja atateuliwa na Chelsea na mmoja na FC Lenz, wakati Mwenyekiti wa Jopo ni toka CAS.Uamuzi wowote wa CAS unaweza tu kukatiwa rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Uswisi tu na si pengine popote.

No comments:

Post a Comment