Monday, August 17, 2009

Zombe na wenzie kuachiwa uhuru...!!!

Abdallah Zombe

Jaji Salum Masatti wa Mahakama Kuu, leo mchana amemwachia huru mkuu wa zamani wa upelelezi mkoani Dar es Salaam, Abdallah Zombe na polisi wengine wanane ambao kwa pamoja walikuwa wanakabliwa na mashtaka ya kuwaua kwa makusudi wafanyabiashara ya madini kutoka, Mahenge mkoa wa.Morogoro na dereva wa teksi wa mkazi wa Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo, ambayo ilikuwa ikivuta watu wengi kwenye chumba cha Mahakama Kuu jijini Dar es salaam, Jaji Masatti amewaachia huru washtakiwa hao baada ya kesi hiyo kuunguruma toka ilipoanza kusikilizwa kwa mara ya kwanza Mei 28, 2008.

Zombe na wenzake walikuwa wanatuhumiwa kuwaua kwa kukusudia Sabinus Chigumbi, maarufu kama Jongo na ndugu yake Ephrahim Chigumbi na Mathias Lunkombe ambao ni wafanyabiashara wa Mahenge. Mwingine ni dereva teksi wa Manzese jijini Dar es salaam, Juma Ndugu.

Inadaiwa kuwa watu hao waliuawa kwa kupigwa risasi kwenye msitu wa Pande ulioko Mbezi Luisi wilayani Kinondoni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Watu hao walikamatwa na polisi kwa madai ya kuhusika kwenye tukio la ujambazi jijini Dar es salaam, lakini gazeti hili likaripoti baadaye kuwa waliouawa hawakuwa majambazi baada ya kuzungumza na watu wa sehemu mbalimbali, zikiwemo Mahenge na Sinza.

Taarifa hiyo ilisababisha Rais Jakaya Kikwete kuunda tume iliyoongozwa na Jaji Kipenka Mussa ambayo uchunguzi wake ulisababisha kutiwa hatiani kwa watu hao na kufunguliwa kesi.

Hukumu ya leo ya Jaji Masatti inaweza kuamsha vilio au vicheko atakapoamua kuwatia hatiani askari hao wa Jeshi la Polisi au kuwaachia huru baada ya kujenga msimamo kutokana na ushahidi uliowasilishwa na pande zote pamoja na maoni ya wazee wa baraza.

Lameck Mlacha, msajili namba mbili wa wilaya wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, aliiambia Mwananchi kuwa siku ya hukumu mahakama itaweka vipaza sauti ili wananchi wanaotarajiwa kufurika mahakamani hapo, kusikiliza hukumu hiyo vizuri.

Pia alisema ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata ujumbe kamili na kuuelewa, hukumu itasomwa kwa lugha ya Kiswahili.

Hali ya ulinzi pia ni miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kuimarishwa mahakamani hapo ili kuhakikisha kuwa mambo yote yanakwenda sawa na kwa amani bila vurugu yoyote.

Awali washtakiwa kwenye kesi hiyo walikuwa 12, lakini baada ya kumalizika kwa hatua ya awali, washtakiwa tisa walionekana wana kesi ya kujibu wakati watatu waliachiawa huru.

Walioachiwa huru ni aliyekuwa mshtakiwa wa sita, Koplo Morris Nyangelela, Koplo Felix Cedrick, aliyekuwa mshtakiwa wa nane na PC Noel Leonard ambaye alikuwa mshtakiwa wa nne.

Hadi sasa Saadi Alawi, ambaye ameelezwa kuwa ndiye aliyetekeleza mauaji hayo kwa kuwapiga risasi watu hao, hajakamatwa.

Zombe, ambaye ni mshtakiwa wa kwanza na ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya Kamanda wa Polisi wa Dar es salaam wakati wa mauaji hayo, alipata ahueni baada ya kusikiliza maoni ya Wazee wa Baraza.

Katika maoni waliyotoa Juni 26, wazee hao walieleza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka bila kuacha mashaka dhidi yake.

Wazee hao walidai kuwa kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na mashahidi 37 upande wa mashtaka, hakuna shahidi hata mmoja aliyeweza kuithibitishia mahakama kuhusika kwa Zombe katika mauaji ya wafanyabiashara hao kwa kuwa hakuna shahidi hata mmoja aliyeieleza mahakama kuwa alimuona Zombe katika eneo la mauaji au hata walikokamatwa Sinza.

"Ili mtu atiwe hatiani kwa kosa kubwa kama hili la mauaji ni lazima upande wa mashtaka uthibitishe bila kuacha shaka kuwa mshtakiwa huyo alifanya kosa hilo. Upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha hatia ya mauaji kwa mshtakiwa wa kwanza" alisema Mzee Kimolo na kuungwa mkono na wenzake.

"Mheshimiwa Jaji, maoni yangu na mapendekezo yangu ni kwamba mahakama yako tukufu imuone mshtakiwa wa kwanza kuwa hana hatia na imwachie huru."Lakini wakati wa kufanya majumuisho Juni 25, upande wa mashtaka uliiomba mahakama imtie hatiani afisa huyo mwandamizi wa polisi kwa kushiriki kosa baada ya kosa (accessory after the facts).

"Kama mahakama itaona kuwa mshtakiwa wa kwanza (Zombe) na wa 13 (Gwabisabi) hawakushiriki katika mauaji kwa kuwa ushahidi ulioko mahakamani hawakwenda Pande, basi iwatie hatiani kwa kosa la Accessory after the facts chini ya kifungu cha 213,387(i) na 388 cha Penal Code," alidai Mtaki.

Mtaki aliileza mahakama kuwa kila kesi huamuliwa kwa mazingira yake na kuitaka mahakama kuzingatia mazingira ya kesi hiyo, ambayo alisema kuwa washtakiwa wote ni askari polisi, baadhi yao wakiwa ni maofisa na wapelelezi walio na uzoefu.

"Kwa hali hiyo shauri hili linapaswa lipewe mtazamo wa kipekee kabisa kwa kuzingatia ushahidi wa pande zote na hatimaye mahakama yako tukufu iweze kufikia uamuzi wa haki ambao sisi tunaamini kuwa washtakiwa wote wana hatia ya mashtaka haya," alisisitiza Mtaki.

Sheria inaweza kumtia hatiani mshtakiwa iwapo anabainika kushiriki kosa, kushiriki kosa baada ya kosa na kushiriki kabla ya kosa.Lakini wakati akitoa mwongozo, Jaji Masatti alisema ingawa sheria inaweza kumtia mtu hatiani kwa kushiriki kosa baada ya kosa, hilo linaweza kutendeka iwapo alishtakiwa kwa kosa hilo.

Wote tisa wameshtakiwa kwa kosa kubwa la mauaji, na wala si kula njama za kuua, jambo ambalo linafanya Zombe awe anatarajiwa kuachiwa huru iwapo hataonekana na hatia ya kushiriki kuua.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa rasmi katika Mahakama hiyo mbele ya Jaji Masatti wakati huo akiwa Jaji Kiongozi Mei 26 mwaka 2006, na jumla ya mashahidi 37 walitoa ushahidi mahakamani hapo kabla ya washtakiwa kusimama kizimbani na kujitetea.

Washtakiwa wengine waliobakia katika kesi hiyo baada ya watatu kuachiwa na mmoja, Koplo Rashid Lema kufariki dunia Aprili 3 mwaka huu, ni SP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, WP 4593 PC Jane Andrew, CPL Emmanuel Mabula, PC Michael Sonza, CPL Ebeneth Saro, C/CPL Rajab Bakari na D/CPL Festus Gwabisabi.

No comments:

Post a Comment