Sunday, August 9, 2009

Hillary Clinton aionya Eritrea


Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bi Hillary Clinton ameonya kuwa Marekani itachukua hatua kali dhidi ya Eritrea iwapo haitaacha kuwasaidia wapiganaji wa Somalia.

Bi Clinton alisema baada ya kufanya mazungumzo na rais wa Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed mjini Nairobi Kenya, kuwa vitendo vya Eritrea ''havikubaliki''.

Amesema pia kuwa Marekani itaongeza nguvu kuisadaia serikali ya umoja ya Somalia.

Eritrea inakanusha kukisadia kikundi cha wapiganaji cha Somalia al-Shabab ambao wanajaribu kuiondoa serikali ya Somalia.

Kundi la al-Shabab linaongezeka nguvu na wasomali laki mbili na hamsini elfu wameyakimbia makazi yao kufuatia mapigano kati ya wapiganaji hao na majeshi ya serikali katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Akiwa katika siku ya pili ya ziara yake barani Afrika, Bi Clinton alikuwa anafanya mazungumzo na kiongozi anayeungwa mkono na Umoja wa Mataifa, muislamu mwenye msimamo wa kati.

Kwa hakika iwapo Al-Shabab wanapata hifadhi nchini Somalia ambapo itakaribisha al-Qaeda na vitendo vya kigaidi, basi itakuwa ni tishio kwa Marekani.

Katika mkutano wa pamoja na rais wa Somalia, Bi Clinton alisema: ''Ni kipindi kirefu kimepita sasa ambapo Eritrea inapaswa kuacha na kukoma kukisaidia kikundi cha al-Shabab na kuanza kuwa msaada na sio kuvuruga amani ya nchi jirani.

''Tunaweka bayana kabisa kuwa vitendo vyao havikubaliki''. Tunakusudia kuchukua hatua kali iwapo vitendo hivyo havitakoma.''

Aliongeza: ''Hakuna shaka kuwa al-Shabab wanataka kudhibiti Somalia na kuitumia kama kituo ambacho watakuwa wakiendesha shughuli zao na hata kujipenyeza nchi jirani na kisha kufanya mashambulio dhidi ya nchi za mbali na karibu.''

Bi Clinton amesema iwapo al-Shabab watapata hifadhi nchini Somalia ''itakuwa ni tishio kwa Marekani.''

Marekani imefutilia mbali uamuzi wake wa kutuma majeshi yake kupigana na waasi nchini Somalia.

Eritrea imekuwa ikikanusha mara kwa mara kukisaidia kikundi cha al-Shabab, ikisema kuwa tuhuma hizo ni za kutengenezwa na kitengo cha usalama cha Marekani.

Kabla ya mazungumzo hayo siku ya Alhamis, Bi Clinton aliwakumbuka waathirika wa milipuko ya mabomu ya mwaka 1998 katika balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya, katika sherehe za kuweka mashada ya maua zilizofanyika mjini Nairobi.

Zaidi ya watu 220 waliuawa na wengine 5000 walijeruhiwa katika shambulio hilo la kwanza lililofanywa na al-Qaeda dhidi ya Marekani.

Shirika la habari la AP limemkariri Bi Clinton akisema kuwa eneo hilo la ubalozi linakumbusha kuwa '' tishio la ugaidi ambalo haliheshimu mipaka, rangi, kabila au dini bado lipo, na linalenga kuharibu na kuwanyima watu nafasi ya kufanya maamuzi yao wenyewe na kuendelea kuishi.''

Kuna taarifa kuwa al-Shabab kikundi cha kiislamu chenye kupendelea sheria kali ya kiislamu na kinachohusishwa na al-Qaeda, kinapata msaada kutoka wapiganaji duniani kote.

Mapema wiki hii polisi nchini Australia iliwakamata watu kadhaa na kuwashitaki kwa kupanga kufanya mashambulio ya kujitoa mhanga mjini Sydney na kusema kuwa watu hao wana uhusiano na al-Shabab.

Mwandishi wa BBC aliyeko Nairobi Will Ross anasema rais wa Somalia anahitaji kila msaada unaopatikana. Vikundi vya kijeshi vinavyounga mkono serikali vinadhibiti sehemu ndogo tu ya makao makuu ya Somalia,Mogadishu.

Anadokeza kuwa ni eneo la hatari sana kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuweza kuingia Somalia, kwani mapigano bado yanaendelea.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia ameiambia BBC kuwa kitendo cha Marekani kuiunga mkono serikali ya Somalia ni ''jambo la msingi sana.''

''Ni wazi kabisa kuwa watu wa Somalia wamechoka, wamekinaishwa na kuchoshwa na vurugu,''. Alisema.

Marekani inakiri kuwa imetoa msaada wa tani 40 za silaha na risasi kwa vikosi vinavyounga mkono serikali ya Somalia mwaka huu, na kwamba inatarajia kupeleka shehena zaidi, anasema mwandishi wetu. www.bbc.com/swahili

No comments:

Post a Comment