Sunday, August 9, 2009

Magaidi wahukumiwa kifo India


Mahakama nchini India imetoa hukumu ya kifo kwa watu watatu waliofanya mashambulio ya mabomu yaliyoua watu 50 mjini Mumbai (bombay) mwaka 2003.

Haneef Sayyed na mkewe Fahmeeda na Ashrat Ansari walipatikana na hatia ya kufanya njama na kuua kwa kukusudia mwezi uliopita.

Milipuko hiyo iliyotokea katika katika eneo la lango kuu la India na katika soko la vito vya dhamani, yalisababisha maafa makubwa na kulitikisa taifa la India.

Wanasemekana kuwa walikuwa wakilipiza kisasi juu ya vifo vya waislamu wakati wa maandamano katika jimbo la Gujarat yaliyotokea mwaka mmoja kabla.

Mamia ya watu wameuawa katika mashambulio kadhaa mjini Mumbai katika miaka ya hivi karibuni.

Watu hao watatu wameonekana kuwa na mahusianao na kikundi cha wapiganaji wa kiisalmu nchini Pakistan, kijulikanacho kama Lashkar-e-Taiba, ambacho wachunguzi wanaamini kilihusika na mashambulio ya Mumbai mwezi Novemba mwaka 2008.

Uhusiano na Pakistan

Katika mahakama maalum inayohusika na kesi za kigaidi, Jaji Puranik aliamuru kwamba watu wote hao watatu waliopatikana na hatia kuwa ni ''lazima wanyongwe hadi kufa''.

Huku wakiwa wamesimama kizimbani watu hao hawakuonyesha kuwa na hisia yoyote wakati hukumu hiyo ikitolewa, mwandishi wa shirika la habari la AFP
anaarifu.

Wanasheria wao wamedokeza kuwa watu hao watakata rufaa juu ya hukumu hiyo ya kifo, ambayo ni mara chache sana kutolewa nchini India, na mara nyingi haitekelezwi au hupunguzwa na rais, shirika hilo linasema.

Mwanasheria wa Haneef Sayyed amesema mteja wake lazima afungwe maisha bila kufikiriwa kupewa msamaha, wakati mwansheria wa Fahmeeda Sayyed amepinga hukumu hiyo ya kifo akisema alikuwa ni mwanamke masikini, asiye na elimu na aliyelazimishwa kufanya uhalifu huo na mumewe.

Mwanasheria wa Ansar Sushan Kunjuramaran hakutoa maombi yoyote sipokuwa Ansar mwenyewe alimwambia jaji kuwa hakubaliani na uamuzi huo wa mahakama.

Mwendesha mashitaka mkuu Ujiwal Nikam amesema uhalifu huo wa watu hao watatu umeonyesha ukatili wa hali ya juu na umesababisha mauaji ya watu wengi wasio na hatia.

''Itakuwa ni kufanyia mzaha mfumo wa sheria na haki iwapo hukumu ya kifo haitatolewa,'' alisema kabla ya hukumu.

Milipuko hiyo ya magari mawili ya mwezi August mwaka 2003 yalileta taharuki katika lango kuu la India na katika soko la Zaveri Bazaar karibu na hekalu la Mumba Devi katika makao makuu ya Mumbai.

Takribani watu 180 walijeruhiwa katika mkasa huo.

Washitakiwa hao watatu wote kutoka Mumbai walifunguliwa mashitaka chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya India ambayo toka wakati huo imetenguliwa.

Watu wengine wawili zaidi Mohammed Ansari na Mohammed Hasan walishitakiwa
lakini waliachiliwa kufuatia marudio ya kesi yao na mahakama maalum mwaka jana.

Washitakiwa hao watuatu walipatikana na hatia ya kupanga milipuko ya mabomu kwa kushirikiana na kundi la Lashkar-e-Taiba.

Kundi la Lashkar linatuhumiwa kufanya mashambulio mengine kadhaa nchini India katika miaka ya hivi karibuni, ikijumuisha ya silaha za bunduki na mabomu mjini Mumbai Novemba mwaka jana.

Hofu ya wapiganaji

Jaji amesema kuwa washitakiwa wote watatu ni wafuasi wa kundi la Lashkar, shitaka ambalo walilikana.

Lashkar ni moja kati ya makundi hatari yanayohofiwa kupigana dhidi ya ngome ya India eneo la Kashmir.

Lilipigwa marufuku nchini Pakistan mwezi Januari mwaka 2002 kufuatia mashambulio ya tarehe 11 mwezi Septemba nchini Marekani.

Hadi wakati huo Lashkar walikuwa wanaweza kufanya shughuli zao kwa uwazi ndani ya Pakistan ikiwemo kachangisha fedha na kuandikisha wafuasi.

Lashkar ilishutumiwa na India kwa mashambulio ya mabomu mjini Delhi mwezi October mwaka 2005 yaliyouwa zaidi ya watu 60 na ya Decemba mwaka 2001 kuvamia bunge la India.

Wachunguzi wa India wanalihusisha kundi hilo na mashambulio ya Mumbai mwezi Novemba mwaka 2008 ambapo watu wenye silaha waliwaua watu wapatao 166 katika mkasa wa siku tatu mfululizo.

Mshambuliaji pekee anayeaminika bado kuwa hai, Mohammad Ajmal Amir Qasab, alikiri kushiriki katika shambulio hilo katika kesi yake nchini India mwezi uliopita.

Naye pia angeweza kuhukumiwa kifo iwapo kukiri kwake kungekubalika na kisha majaji kutoa hukumu ya juu zaidi.

Habari zaidi zinasema kuwa, Pakistani imeomba polisi wa kimataifa kutoa tahadhari kote duniani juu ya watu wapatao 13 kuhusiana na uchunguzi wa mashambulio ya mwaka 2008.

No comments:

Post a Comment